Skip to content

Mwakilishi wa kike kaunti ya Marsabit Naomi Jillo akosoa ujenzi wa kambi ya usalama eneo la Tiitu

Mzozo wa umiliki wa ardhi kwenye mpaka wa kaunti ya Marsabit na Wajir unaendelea kuibua hisia tofauti huku viongozi na wazee wa jamii ya kaunti ya Marsabit wakikashfu ujenzi wa kambi ya usalama katika eneo la Tiitu kwenye mpaka wa kaunit hizo mbili.

Mwakilishi wa kike kaunti ya Marsabit, Naomi Jillo Waqo ambaye alizuru eneo hilo alisikitika kuona kwamba ujenzi wa kituo hicho unaendela licha ya waziri wa usalama wa ndani, Kipchumba Murkomen kuahidi kusitishwa wakati wa mswada maalumu bungeni kujadili swala hilo wiki jana.

Waqo alimshutumu mbunge wa Eldas Adan Keynan akidai kuwa anatumia ushawishi wake wa kisiasa kushinikiza ujenzi wa kituo hicho kwa ardhi inayozozaniwa huku akitoa wito kwa rais Dokta William Ruto kuingilia kati na kuhakikisha wazee wawili waliokamatwa wanaachiliwa huru na haki kutendeka.

Nao wazee wa jamii ya Borana kutoka eneo bunge la Moyale pia wametaka kuachiliwa mara moja kwa aliyekuwa chifu wa Sololo, Dabasa Dambi, pamoja na mzee Guracha Dambala ambao walikamatwa kwa kuhusishwa na mzozo huo.

Mahakama ya Kahawa jijini Nairobi iliamru wawili hao kuzuiliwa kwa muda wa siku 10, kuruhusu uchunguzi kukamilika kwa madai ya wawili hao kuhusishwa na kundi la Oromo Leberation Army (OLA).

Wakizungumza na vyombo vya habari katika eneo la Dambalafachana kaunti ya Marsabit, wazee hao wakiongozwa na mzee Hajj Hussein Kadida, wametaka suluhu kuafikiwa kuhusiana na mzozo huo na haki kutendeka.

Siku ya Jumatano gavana wa kaunti ya Marsabit, Mohamud Mohammed Ali alishiriki mazungumzo na waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen afisini mwake huku Murkomen akieleza kuwa mazungumzo hayo yaliangazia zaidi maendeleo, usalama na uwiano katika kaunti ya Marsabit.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *